Dodoma – Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) leo inaanza kuwahoji watu mbalimbali waliohusika katika uchunguzi au tuhuma za kashfa ya IPTL kuhusu uchotaji wa Sh306 bilioni katika akaunti ya Escrow iliyoko katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Jukumu hilo linaanza baada ya juzi kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe kukabidhiwa vitabu vitano vya ripoti hiyo na Naibu Spika, Job Ndugai na kuagizwa kuipitia na kutoa mapendekezo katika kila hadidu ya rejea.

magic replica watches

Zitto alipoulizwa kamati inaanzia wapi, alijibu kwa kifupi kuwa itaanza kuwahoji Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Bila kufafanua alisema tayari viongozi hao wamepewa hati za wito kuwataka kufika mbele ya kamati.

Kamati hiyo inayokutana kwa siku 10, inatakiwa kuwasilisha ripoti yake bungeni Novemba 26, mwaka huu ambako itajadiliwa kwa siku moja, muda ambao baadhi ya wabunge wamesema hautatosha.

Muda Zaidi

Kwa kile kinachoelezwa kuwa uchunguzi huo unahusu watu wazito wakiwamo mawaziri, watendaji wazito wa Serikali na wabunge, Bunge limeelezwa kuwa muda uliotengwa kujadili hautatosha.

Ombi hilo lilitolewa jana na Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde aliyeomba mwongozo wa Spika akihoji kwa nini Kamati ya Uongozi isiongeze muda ili wabunge waweze kujadili vya kutosha ripoti hiyo.

“Ratiba inaonyesha tarehe 27 ndiyo tutajadili ripoti hiyo baada ya PAC kuiwasilisha. Kwa nini Kamati ya Uongozi isiongeze muda ili watu waweze kuijadili kwa muda mrefu kwa kuwa katika ripoti hiyo kuna baadhi ya mawaziri, viongozi na wabunge wanaolalamikiwa?” aliuliza Lusinde na kuongeza:

“Kama kikao cha jana (juzi) mliahirisha Bunge mchana na jioni hakukuwa na kikao kwa nini huo muda usiongezwe kwenye mjadala wa ripoti hiyo?”

Alisema kuna uzoefu kwamba mtu anayelia sana kwenye msiba ndiye aliyeua, hivyo ni muhimu muda ukaongezwa ili mjadala huo upate nafasi yake. “Tunaomba muda wa kujadili hili jambo kwa urefu ili tuondoe mazingezinge haya,” alisema Lusinde.

Akijibu mwongozo huo, Naibu Spika, Job Ndugai alisema ushauri huo wa Lusinde ni mzuri na Kamati ya Uongozi itaufanyia kazi itakapokutana.

Kauli ya Lusinde inaashiria kuwa baadhi ya wabunge wameanza kunusa kuwa matokeo ya ripoti hiyo yanaweza kusababisha mtikisiko wa tano katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Ripoti hiyo inatokana na uchunguzi maalumu wa CAG kuhusu fedha hizo zilizochotwa katika akaunti ya Escrow ndani ya BoT, zilipokuwa zinatunzwa zikiwa gharama za uwekezaji (capacity charge) kwa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL baada ya kutokea mgogoro wa kibiashara baina yake na Tanesco.

Tanesco ililalamika kuwa ilikuwa inailipa zaidi IPTL kinyume na gharama za uwekezaji, hivyo kuamuliwa na Mahakama kuwa fedha ilizokuwa inatakiwa kulipa ziwekwe katika Escrow hadi upatikane ufumbuzi wa mgogoro huo.

Hata hivyo, kesi hiyo ilipohukumiwa Februari 12 mwaka huu, ikibainisha kweli Tanesco ilikuwa inailipa zaidi IPTL, tayari fedha zilizokuwa katika akaunti hiyo zilishachotwa na IPTL kwa ruksa ya baadhi ya viongozi wa Serikali.

Ripoti hiyo inaweza kuondoka na vigogo waliohusika na kashfa hiyo kama ilivyowahi kutokea katika kashfa nyingine nne zilizoitikisa Serikali ya Awamu ya Nne za EPA, Richmond, Tokomeza Ujangili na Ukaguzi wa CAG.

Previous articleLady Jaydee
Next articleZiara Ya Rais Wa China Nchini Tanzania Yatumika Kusarisha Meno Ya Tembo