Dar es Salaam – Ziara ya Rais Xi Jinping wa China aliyoifanya nchini Machi mwaka jana, imezua kizaazaa na kuitia ila sifa ya Tanzania kimataifa, baada ya maofisa waliokuwa wameambatana naye kuhusishwa na biashara haramu ya meno ya tembo.

Ripoti iliyotolewa na taasisi ya kimataifa ya Uingereza inayojihusisha na uchunguzi wa masuala ya mazingira, inadai kuwa maofisa hao walinunua kiasi kikubwa cha bidhaa hizo katika soko la Mwenge, Dar es Salaam, kisha kuzisafirisha kidiplomasia kwa ndege ya rais huyo.

Taasisi hiyo iitwayo Environmental Investigation Agency (Wakala wa Uchunguzi wa Mazingira– EIA), katika ripoti hiyo inasema maofisa hao walitumia fursa ya kidiplomasia ya kutokukaguliwa kwa mizigo yao, kupitisha bidhaa hizo haramu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA).

Biashara ya meno ya tembo ilizuiwa kimataifa tangu mwaka 1989 kwa kusainiwa kwa azimio la kulinda viumbe walio hatarini (Cites), azimio ambalo pia limesainiwa na China na Tanzania.

Taarifa hiyo iliandikwa kwa mara ya kwanza jana na Gazeti la New York Times la Marekani na baadaye kuwa moja ya habari zilizopewa uzito wa juu katika vyombo vingine vya habari vya kimataifa, huku Kituo cha Televisheni cha Shirika la Habari la Uingereza BBC, kikijadili kwa kina kashfa hiyo iliyopewa jina la “ndege ya rais kutumika kusafirisha meno ya tembo”.

BBC katika taarifa yake ilitumia picha za meno ya tembo na zile za maktaba ambazo zilikuwa zikimwonyesha Rais Jinping akilakiwa na Rais Jakaya Kikwete pamoja na viongozi wengine wa Tanzania alipowasili nchini kwa ziara hiyo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema jana kwamba Serikali haifahamu chochote kuhusu tuhuma hizo na kwamba hata kama zingekuwa na ukweli ndani yake waliopaswa kuulizwa ni Serikali ya China.

“Serikali haina evidence (ushahidi) wowote unaoonyesha kwamba suala la aina hii lilitokea, lakini pili mimi siamini kama kweli maofisa wa China walifanya kitendo hiki na kama hicho kilifanyika basi wanaopaswa kuulizwa ni Serikali ya China,” alisema Balozi Sefue na kuongeza:

“Siamini kama madai hayo ni ya kweli kwa sababu maofisa wanaosafiri na viongozi hukaguliwa, kwa nini wasikaguliwe na China ni marafiki zetu wazuri tu? Kwa hiyo sisi kama Serikali hilo jambo hatulifahamu kabisa.”

Baada ya kutangazwa katika vyombo vya habari vya kimataifa, maofisa wa Serikali ya China wamekanusha tuhuma hizo wakisema, “hazina ukweli wowote” wala ushahidi wa kuzithibitisha.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa China, Hong Lei alinukuliwa na Shirika la Habari la Associated Press (AP) akisema: “Ripoti hiyo haina ushahidi wowote na hatukufurahishwa kabisa na taarifa hizi.”

Mkurugenzi wa usafirishaji wa viumbe walio kwenye hatari ya kutoweka nchini China, Meng Xianlin alipuuza madai hayo akisema: “Tuhuma pasipo ushahidi haziwezi kuaminika.”

Ununuzi wa nyara

Ripoti hiyo inayoitwa “Wanatoweka: Uhalifu, Rushwa na Kuangamizwa kwa Tembo wa Tanzania,” inadai kuwa ujumbe wa maofisa wa Rais Jinping ulifika nchini wiki mbili kabla ya ujio wa Rais huyo na kununua pembe za ndovu katika eneo la Mwenge ambalo ni maarufu kwa uuzaji vinyago.

Inadai kuwa ujumbe huo ulinunua meno ya tembo kwa Dola za Marekani 700 (sawa na Sh1,120,000) kwa kilo moja, bei ambayo ni mara mbili ya ile ya kawaida na kwamba Wachina hao walinunua maelfu ya kilo za meno hayo na kuyasafirisha kwa ndege ya Rais Jinping.

Mfanyabiashara katika eneo hilo, aliyetambulika kwa jina moja la Suleiman amenukuliwa katika ripoti hiyo akisema bei ya meno ya tembo ilipanda kutokana na kuongezeka kwa mahitaji yake wakati wa ziara hiyo.

Mtu mwingine ambaye hakutajwa jina lake katika ripoti hiyo anaeleza kuwa jambo hilo lilifanyika pia hata wakati wa ziara ya aliyekuwa Rais wa China, Hu Jintao mwaka 2009 ambako maofisa waliokuwa katika msafara huo walinunua bidhaa hizo.

“Wanakuja kuchukua vitu vingi, si kwa ajili ya Hu Jintao, bali kwa ajili yao. Baada ya hapo wanakwenda uwanja wa ndege na kupita bila kukaguliwa kwa sababu VIP hawakaguliwi,” alidai.

EIA katika taarifa hiyo pia inadaiwa kuwa Wanadiplomasia wa China pamoja na maofisa usalama wa nchi hiyo kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa wa Tanzania walifanikisha upatikanaji na usafirishaji wa meno ya tembo kwenda China.

“Tanzania ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa kutoa meno ya tembo kwa wingi. Pia China ndiyo mnunuaji mkubwa wa meno ya tembo duniani,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo yenye kurasa 36.

Inadai kuwa katika kipindi cha miaka minne iliyopita, Tanzania imepoteza tembo wengi kutokana na ujangili kuliko nchi yoyote duniani. EIA inafafanua kuwa zaidi ya tembo 10,000 waliuawa mwaka 2013 pekee, ukiwa ni wastani wa tembo 30 kwa siku.

Ripoti hiyo inasema tembo wengi wanaouawa ni wale waliopo katika Pori la Akiba la Selous ambako idadi yake imepungua kutoka 39,000 waliokuwapo mwaka 2009 hadi 13,000 mwaka jana, idadi ambayo ni ya chini kabisa katika kipindi cha zaidi ya miaka 10 iliyopita.

Ripoti hiyo inasema kuwa wakati Rais Kikwete akiingia madarakani mwaka 2005, Tanzania ilikuwa na tembo 142,000, lakini kutokana na kasi ya matukio ya ujangili, inakadiriwa kuwa wanyama hao watakuwa 55,000 tu wakati atakapokuwa akimaliza uongozi wake mwakani.

Tofauti na nchi nyingine za Kiafrika, ripoti hiyo inaeleza kuwa ujangili nchini unafanyika kirahisi na kwa kasi kubwa kutokana na amani iliyopo, tofauti na nchini nyingine kama Jamhuri ya Afrika ya Kati na Kenya ambako kumekuwa na mapigano ya mara kwa mara baina ya vikundi pamoja na uwepo wa makundi ya ugaidi ambayo pia huendesha biashara hiyo haramu kwa kuua tembo.

Vitendo vya rushwa

Ripoti hiyo inafafanua kuwa tatizo la ujangili nchini linasababishwa na kuongezeka kwa vitendo vya rushwa, udhaifu wa kiutawala na vitendo vya kihalifu vinavyozidi kuongezeka siku hadi siku.

Hoja hiyo inathibitishwa na ukweli kwamba 2013, Tanzania iliporomoka kwenye viwango vya kimataifa vya udhibiti rushwa kwa kushika nafasi ya 111 kati ya nchi 177, huku ikishika nafasi ya 15 katika viwango vya utawala bora barani Afrika na kuwa nchi pekee iliyoshuka katika miaka mitano iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulika na Dawa na Uhalifu (UNODC) iliwahi kubainisha kuwa rushwa ni kikwazo kikubwa katika utawala bora Tanzania.

Rushwa ndiyo inaelezwa kufanikisha mchakato mzima wa ukusanyaji na usafirishaji wa meno ya tembo, huku askari wanyamapori wakitajwa kusaidia kutoa taarifa za yaliko makundi ya tembo kwa majangili.

Ripoti hiyo pia inawataja polisi kuhusika kwa kukodisha silaha na kusaidia usafirishaji wa meno ya tembo ili yasikamatwe huku maofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakidaiwa kuruhusu makontena yaliyobeba meno ya tembo kupita bandarini kwenda nje ya nchi.

Msemaji wa Polisi, Advera Bulimba alikataa kuzungumzia tuhuma zilizoelekezwa kwa polisi katika ripoti hiyo mpaka pale atakapoiona na kuisoma.

“Siwezi kusema chochote kuhusu ripoti hiyo. Ilete ofisini kisha tuijadili mimi na wewe, vinginevyo siwezi kuzungumzia kitu ambacho sijakiona,” alisema na kuongeza kuwa ripoti nyingine zinakuwa hazina weledi katika tafiti zake.

Ripoti hiyo inasema mwaka 2012, kuna taarifa kwamba Rais Kikwete alikabidhiwa orodha ya majina ya watu ambao walibainika kuhusika katika ujangili na kwamba wengi walikuwa wafanyabiashara wakubwa na viongozi CCM.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa watu wengi katika orodha hiyo hawakuchunguzwa wala kuchukuliwa hatua zozote na kwamba hiyo ni dalili ya udhaifu wa kiutawala katika kufanya uamuzi.

SOURCE: Mwananchi

Previous articleVigogo Takukuru, TRA, CAG, Kikaangoni Kamati Ya Zitto
Next articleMabasi Yagongana Mkoani Mara Nchini Tanzania na Kusababisha Vifo Vya Watu 39