Linapotajwa jina lake,kwa hakika hustua nyoyo za watu wengi duniani hasahasa wapenzi wa muziki wa taarab kisiwani Zanzibar na duniani kwa ujumla. Alivuna umaarufu mkubwa na kumfanya kuwa kipenzi cha watu duniani kote kwa uwezo wake mkubwa na wakipekee kwa kuimba,kupigangoma na kumiliki jukwaa licha ya umri wake kuwa mkubwa mno.

Jambo hili lilimfanya aweke historia kubwa duniani, kutokana na kwamba mpaka sasa haikuwahi kutokea mwanamuziki aliyekuwa na umri kama wake kuweza kufanya aliyoyafanya Bi kidude.

Marehemu Bi Kidude enzi za uhai wake.

Jina lake halisi ni Fatuma Binti Baraka, inakadiriwa kua alizaliwa mnamo mwaka 1910 katika kijiji kilichoitwa Mfagimalingo mjini Unguja. Bi kidude mara kadhaa alipokua akiulizwa kuhusu mwaka aliozaliwa, alisema kwamba amezaliwa zama za Sarafu ya Rupia, iliyokua ikitumika Afrika Mashariki mnamo miaka ya 1910.

Mnamo mwaka 1920 akiwa binti mdogo, alikua akiimba katika matamasha ya kiutamaduni kisiwani Zanzibar. Aliibuka na kuwa maarufu sana tangia akiwa mdogo kwa umahiri wake wa kuimba na kutunga mashairi ya nyimbo za taarab kisiwani Zanzibar. Kutokana na uwezo wake ilimfanye awe mwimbaji wa kwanza wa kike kutoka Zanzibar.

Bi Kidude enzi za ujana wake.

Alipofikisha umri wa miaka 13, wazazi wake walimtafutia mume na kumlazimisha aolewe, jambo ambalo Bi kidude hakukubaliana nalo na kumfanya atoroke kisiwani Zanzibar na kukimbilia Tanzania bara. Mnamo mwaka 1940, alirejea kisiwani Zanzibar na kuishi katika nyumba yake akiwa huru na kuendeleza shughuli zake za muziki. Aliendelea kufanya ziara mbalimbali Afrika mashariki.

Bi kidude alikua na ujasiri wa hali ya juu kwani alikua akivuta sigara na kunywa pombe, licha ya kuwa jambo hilo lilikuwa kinyume na utamaduni wa jamii ya watu wa Zanzibar. Kulingana na tamaduni za Kisiwani humo ilikua hairuhusiwi kwa mwanamke kunywa pombe wala kuvuta sigara.

Bi kidude akijiburudisha kwa Sigara.

Mbali na kuwa hodari katika utunzi wa mashairi na uimbaji pamoja na uwezo wa kumiliki jukwaa, Bi Kidude alikua na uwezo mkubwa wa kupiga ngoma, hali iliyowashangaza watu wengi kwa uwezo mkubwa na wa kipekee.

Bi kidude akionyesha umahiri wa kupiga ngoma.

Kwa maelezo yake Bi kidude aliwahi kuweka wazi kwamba, alijifunza muziki kupitia kwa mwanamuziki maarufu kipindi hicho aliekua akiitwa Sitti binti Saad. Kutokana na ukaribu uliokuwepo kati ya wawili hawa, ilipelekea Bi kidude kujifunza kuimba taarab. Umahiri na umaarufu wa Sitti bint Saad kisiwani Zanzibar, ulipelekea wageni wengi waliofika kisiwani humo kupata shauku ya kutaka kumuona kila wanapotembelea kisiwa hicho, Bi kidude alikua akiwapokea wageni hao na kuwapeleka moja kwa moja kwa Sitti binti Saad.

Bi Kidude aliwahi kuolewa lakini hakuwai kupata mtoto katika maisha yake yote. Hata hivyo ndoa yake haikudumu kutokana na alichokiita manyanyaso aliyokuwa akiyapata katika ndoa yake. Mnamo mwaka 1930, Bi Kidude aliamua kwenda Misri ambako aliendelea na shughuli za muziki, akiwa huko umahiri wake ulizidi kudhihirika na kumzolea umaarufu zaidi.

Bi Kidude akiwa studio akirekodi moja kati ya nyimbo zake.

Wahenga walisema, mkataa kwao ni mtumwa. Hatimae Bi Kidude alirudi kwao kisiwani Zanzibar mnamo mwaka 1940. Na aliendea kufanya ziara mbalimbali  za kimuziki ndani ya Afrika mashariki. Bi Kidude pia amewahi kufanya ziara katika nchi nyingi ulimwenguni zikiwemo Ufaransa, Ujerumani, Ufini, Hispania na Uingereza.

Mbali na muziki lakini Bi kidude alikuwa akifanya biashara ya kuuza Wanja na Hina. Lakini pia Bi kidude alikua mtaalamu wa tiba za dawa za mitishamba, ambapo watu wengi wenye maradhi mbalimbali walienda kwake kwa matibabu.

Bi Kidude amewahi kujinyakulia tuzo mbalimbali katika muziki, baadhi ya tuzo hizo ni pamoja na tuzo ya ZIFF na tuzo ya WOMAX.
Hakuna kinacho dumu milele, hatimaye wingu la simanzi na majozi lilitawala pale ambapo Malkia huyu wa Taarab alipoaga dunia mwaka 2013 kutokana na maradhi ya Kisukari na uvimbe kwenye kongosho. Daima dunia itamkumbuka na pengo lake halitoweza kuzibika.

Jeneza lililobeba mwili wa marehemu Bi Kidude.

Previous articleMsanii Wa Bongo Flava Amini Avunja Ukimya
Next articleIjue Hifadhi Ya Taifa Ya Serengeti Nchini Tanzania