Rais wa Russia Vladimir Putin, amevipa utayari na kuviweka kwenye tahadhari ya juu vikosi vyake vya kijeshi vinavyotumia silaha za nyuklia. Vikosi hivyo ambavyo kazi yake kubwa ni kusimamia uendeshaji, uboreshaji, na utumiaji wa mabomu ya nyuklia pale tu inapoonekana kama kuna umuhimu wa kutumia silaha hizo.
Hatua hii ya Rais Putin imetafsiriwa na viongozi wengi duniani kuwa ni ya hatari na isiyo na ulazima wowote kwa muda huu.
Rais Putin amesema ameamua kuchukua hatua hii kutokana na matamko mbalimbali ya kutishiwa usalama dhidi ya nchi yake kutokea mataifa makubwa ya Magharibi na NATO. Pia amesema vikwazo vinavyowekwa dhidi ya nchi yake vinamfanya aweke utayari majeshi yake ili kukabiliana na taifa lolote ikiwemo utumiaji wa silaha za nyuklia.
Viongozi mbalimbali kutoka idara ya ulinzi ya Marekani (Pentagon) wamedai, hakuna vitisho vyovyote kutoka Marekani na NATO dhidi ya Russia na hakukuwa na ulazima wowote wa Rais Putin kuchukua hatua hiyo.
Hata hivyo viongozi hao wamesisitiza kuwa Marekani iko tayari kujilinda na kuwalinda washirika wake wa NATO kama kutakuwa na shambulizi lolote kutoka Russia.