Tanzania ni miongoni mwa nchi barani Afrika inayozungukwa na vivutio vingi vya utalii na vingine inawezekana hata havitambuliwi na wenyeji.
Ziwa Ngosi yawezekana kuwa ni miongoni mwa vivutio hivyo.
Ziwa hili ambalo ni la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya ziwa lingine la kreta lililopo Ethiopia linaakisi muonekano wa bara la Afrika katika upande wa kusini, magharibi, kaskazini na mashariki pamoja na visiwa vyake vya Unguja na Pemba.
Ziwa Ngosi linapatikana kwenye milima ya Uporoto, Mkoa wa Mbeya nyanda za juu kusini mwa Tanzania , ziwa hili linatajwa kutokana na mlipuko wa volkano hivyo ni tofauti na maziwa mengine kama ziwa victoria au ziwa nyasa.
Upekee au utofauti wa ziwa hili ni kwamba ziwa hili liko juu ya milima na katikati ya misitu na lina urefu wa km2.5, upana wake ni km 1.5 , kina chake ni mita 74 na lina ukubwa wa hecta 9332.
Muonekano wa bara la Afrika ambao upo katika ziwa la Ngosi ni sawa na mchoro unao onekana wa ramani ya bara la afrika pamoja na visiwa vyake uliopo kwenye jiwe kubwa lililopo mkoani Njombe, Kusini magharibi mwa Tanzania ambao haujachorwa na mwanadamu.
Ramani ya bara la Afrika iliyochorwa kwenye Jabali Njombe Tanzania
Innocent Lupembe ni mtaalamu wa misitu na mali asili katika wakala wa huduma za misitu nchini Tanzania kanda ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania anasema hifadhi ya msitu wa mporoto ulianza kutunzwa mwaka 1937 kwa ajili ya kuhifadhi vyanzo vya maji,mimea pamoja na wanyama.
Msitu huu ni wa kipekee kwa sababu una ziwa ndani yake tofauti na misitu mingine na ili uweze kuliona ziwa ni lazima upande mlima ndio unaweza kuliona.
Ziwa hili halina mto unaoingiza wala kutoa maji, ni sawa na maji kwenye bakuli.
Kima cha maji hakibadiliki
Ujazo wa maji huwa haubadiliki yani huwa hivyohivyo wakati wa masika au kiangazi na ujazo wa maji huwa haubadiliki.
Maajabu mengine katika ziwa hili ni kwamba maji ya Ziwa Ngozi huwa lina muonekano wa rangi tofauti tofauti kila wakati, kuna wakati ukifika unakuta ziwa lina rangi ya samawati , kijani au nyeusi .
Uwepo wa misitu husababisha rangi ya maji kubadilika na upande wa jua linapowaka”Lupembe alieleza .
Ndege hupendelea kuogelea pamoja na aina fulani ya bata huwa wanaogelea humo kwa wingi na kufanya ziwa kuwa na muonekano wa kupendeza zaidi.
Licha ya kuwa ziwa hilo linavutia kuangalia lakini halina samaki wala kuwa na historia ya uwepo wake na vilevile sio rafiki kwa kuogelea.
Mtaalam wa hifadhi hiyo alibainisha kwamba miaka miwili iliyopita ziwa hilo liliweza kusababisha vifo vya watoto wawili ambao walikufa baada ya kujaribu kuogelea lakini kabla ya hapo hakuna mtu aliyeweza kujaribu kuogelea kutokana na eneo hilo kuaminika kiimani.
Lakini kwa sasa serikali ina mpango wa kuanzisha utalii wa kuogelea kwa maboti madogo madogo na kuwekeza zaidi kwa ajili ya utalii.
Serikali ya Tanzania ina mradi mkubwa wa umeme ambao unaendelea ingawa wanachipa nje ya mlima.
Hii ni kutokana kuwa katika ziwa hili kuna joto ardhi na linatoa maji moto kwa chini ingawa ziwa Ngosi lenyewe juu maji ni baridi lakini chini ni moto.
Kuna sehemu kadhaa katika mkoa huo wa Mbeya ambapo maji yanatoka ya moto kabisa mpaka mtu unaweza kuchemsha mayai na chanzo kinatoka katika ziwa ngosi.
Kwa sasa eneo hilo linatembelewa na wageni kutoka nje ya nchi zaidi ya wenyeji na wanafunzi wa shule huwa wanafika hapo kwa wingi kwa ajili ya kujifunza.
Wanakijiji wa eneo hilo wana imani juu ya ziwa ngosi
Mwalingo Kisemba ni chifu ambaye ni diwani katika kata ya Inyala halmashauri ya wilaya ya Mbeya.
Yeye anasema katika kabila la wasafa waliliita ziwa Ngosi au Ligosi kwa sababu waliona ni kubwa sana na kiimani ya kisafa waliamini kwamba Mungu yupo huko na walikuwa wakija kufanya maombi ili mvua inyeshe.
Katika kabila lao, wao waliamini kuwa ni bwawa la ajabu kutokana na maji yake kuwa baridi juu na chini kuwa moto.
Kisemba aliongeza kwamba maji ya ziwa hilo yaliaminika kuwa ni dawa ya ngozi, na watu walikuwa wakipaka wanapona ugonjwa wa ngozi kitu ambacho kuna ambao wanaamini hivyo mpaka leo.
Source: B.B.C