Tume ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imetoa taarifa juu ya haki za binaadamu maeneo mbalimbali duniani na kuonesha wasiwasi wake juu ya hali ya Tanzania.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet ameeleza katika taarifa hiyo kuwa nchini Tanzania kumekuwepo hali ya “kuongezeka kwa ukandamizaji wa kidemokrasia na haki za raia, hali ambayo inazidi kufanya mazingira ya haki za binadamu kuwa duni”. Ameeleza hasa mabadiliko ya sheria mbalimbali hususani (Na. 3) ya 2020, ambayo amesema kuwa inazuia uwajibikaji wa serikali kwa ukiukaji wa haki za binadamu nchini Tanzania.

Kwa ukanda wa Afrika Mashariki taarifa hiyo pia imegusia hali ya haki za binaadamu katika mataifa ya Ethiopia, Somalia na Burundi.

Kamishna amesema nini?

Kamishna Bachelet amesema wakati uchaguzi ukitarajiwa kufanyika mwezi ujao nchini Tanzania, ”tumekuwa tukipokea ripoti kuhusu ukamataji holela na kushikiliwa kwa wanaharakati, waandishi wa habari na wapinzani.

“Kati ya sheria nyingi ambazo zimezuia haki ya raia mitandaoni na nje ya mtandao katika miaka ya hivi karibuni, Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya 2020 inaminya wigo wa kufungua kesi za ukandamizwaji wa haki za binaadamu… kubinywa zaidi kwa haki za binadamu kunaweza kusababisha athari mbaya, na amehimiza hatua za haraka na endelevu kuzuia hali hii,” ameeleza Bi Bechelet.

Pia ametoa wito kwa Serikali kusimamia haki za wakimbizi wote, na kuhakikisha kuwa kurudi kwa wakimbizi kunasimamiwa kwa usalama, kwa heshima na kwa hiari.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) ya 2020 ulipitishwa na Bunge la Tanzania mwezi Juni na baadaye kusainiwa kuwa sheria na rais John Magufuli. ikiwemo kuwapa kinga ya viongozi wakuu akiwemo rais dhidi ya kushtakiwa kwa madai ya kuvunja katiba na sheria.

Kati ya mabadiliko hayo yaliyopitishwa, maeneo mawili yalizua mjadala na kupingwa vikali na wanaharakati wa haki za binaadamu na vyama vya upinzani.

Eneo la kwanza ni la viongozi wakuu wa mihimili ya dola, ambao ni Rais, Makamu wa Rais, Jaji Mkuu, Spika na Naibu Spika kushtakiwa kwa kuvunja sheria na katiba wakiwa madarakani. Kwa mujibu wa sheria hiyo, sasa atakayeshtakiwa kwa niaba ya viongozi wote hao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Eneo la pili ni kuminywa kwa wigo wa kufungua kesi za kikatiba, kabla ya sheria hiyo kupitishwa, mtu yeyote alikuw na uhuru wa kwenda mahakamani na kufungua kesi ya kikatiba pale anapoona jambo fulani hususani la ukiukwaji wa haki za binaadamu linafanyika kwa mujibu wa sheria. Hivi sasa, inahitajika mtu kuwa na maslahi ya moja kwa moja ama kuathirika moja kwa moja na sheria husika kabla ya kufungua kesi.

Hoja za serikali ya Tanzania ni zipi?

Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Palamagamba Kabudi ameiambia BBC kwamba wamepokea ripoti hiyo kwa mshangao mkubwa na kuongeza kwamba kamishena huyo angelikuwa Tanzania hangeliandika maneno kama hayo au kutoa tathmini aliyoitoa.

”Kwanza tumechukua hatua ya leo kwamba balozi wa Tanzani katika Umoja wa Mataifa katika ofisi ya Genive anawasilisha majibu yetu rasmi kuhusu taarifa hiyo aliyoitoa” alisema Bwana Kabudi.

Pia aliongeza kuwa hali halisi nchini Tanzania ni tofauti na yale aliyosema Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Michelle Bachelet akiangazia hali ya siasa kipindi hiki cha uchaguzi.

”Sasa tuko katika uchaguzi mkuu tunao wagombea nafsi ya urais 17 na wote wanafanya mikutano yao nchi nzima kila sehemu na hakuna aliyezuiliwa kufanya mikutano ”anasema” kweli kwa wengine ni mshangao”.

Akizungumza na BBC wakati muswada wa sheria hiyo ukipitishwa Bungeni,Mwanasheria Mkuu wa Tanzania, Profesa Adelardus Kilangi alisema mabadiliko hayo hayataondoa dhana ya kupata suluhu.

“Lengo la kufungua kesi hizi ni kupata suluhu, hivyo hata akishtakiwa mwanasheria mkuu bado suluhu itapatikana mahakamani kisheria.”

Kwa mujibu wa Profesa Kilangi, hata sasa kwenye kesi zote ambazo serikali inashtakiwa ama hata kesi za ubunge bado mwanasheria mkuu anasimama mahakamani.

“Lengo la marekebisho haya pia ni kuwa na maudhui ya dhana ya kinga dhidi ya Rais ambayo ni kulinda hadhi ya Rais na nafasi yake,” amesema pia Profesa Kilangi.

Kuhusu haki ya mtu yoyote kufungua mashtaka ya haki za ukiukwaji wa haki za binadamu, amesema kuwa Katiba inaelekeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kufuatwa utakaowekwa kisheria.

“Hapa hatukiuki katiba, tunaweka utaratibu wa kisheria…hili suala la nani ahusike katika kufungua mashtaka haya (locus standi) ni mjadala mpana. Tunasema yule ambaye mwenye maslahi ya moja kwa moja ndiyo afungue mashtaka. Hata Mahakama ya Haki za Binadamu ya Ulaya imeweka wazi msimamo wake kuwa lazima uwe umeathirika moja kwa moja ndiyo ufungue mashtaka katika mahakama hiyo.”

Somalia

Kuhusu nchini Somalia ripoti imeeleza kuhusu ongezeko la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake, wasichana na wavulana, huku kukiwa uchunguzi mdogo sana .

”Ninatoa wito kwa mamlaka za Somalia kusimamia sheria makosa ya kingono iliyoidhinishwa na baraza miaka miwili iliyopita. ”Nimetiwa moyo na uamuzi wa wiki iliyopita kumteua mwendesha mashtaka maalum kufanya uchunguzi matukio ya mauaji ya wanahabari.

”Ni muhimu mataifa yote yakatambua na kulinda haki ya watu wake kuwa huru kueleza maoni yao, na kuwalinda wanahabari dhidi ya ukamataji kuholela, kushikiliwa kinyume cha sheria, kudhalilishwa, kutishiwa, kushambuliwa na kuuawa” imeeleza ripoti hiyo.

Burundi

Hatua zilizochukuliwa tangu mwezi Julai kuwakamata na kuwashtaki wanachama wa chama tawala tawi la vijana maafisa wa juu wa polisi na viongozi wa serikali za mitaa wanaodaiwa kufanya makosa yauporaji na makosa mengine inatia moyo.

Hata hivyo, tangu mwezi Mei baada ya uchaguzi, Ripoti za UN zinaonesha kuwepo na kukamatwa kwa watu kutokana na sababu za kisiasa, pia kuchomwa kwa nyumba za wanachama wa upinzani. Ninashauri mamlaka kuhakikisha inafuata mchakato wa kufanyika kesi kwa haki , na kusimamia haki za binadamu. Hii ni njia bora zaidi ya kuepuka mzozo”. alisema Michelle Bachelet

Serikali ya Burundi haijapatikana kuzungumzia ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa.

Mataifa mengine yaliyoguswa kwenye ripoti hiyo ni Ethiopia, Mali, Marekani, Saudi Arabia, Ivory Coast, Iran, Iraq, Afghanistan, Colombia, Mexico na Brazil.

Source: BBC

Previous articleTundu Lissu Aomba Mdahalo Na Rais Magufuli | Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020
Next articleVinyl Record Sales Surpass CDs For The First Time Since The 1980s