Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Mhe. Tundu Lissu ametoa wito kwa Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Mhe. John Magufuli, kuwa tayari kushiriki mdahalo utakaowakutanisha wagombea hao wawili ili waeleze na kuhojiwa kuhusu maono na mipango yao ya namna ya kutekeleza agenda zinazohusu Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watanzania, ikiwa ni sehemu ya wapiga kura kuwapima na kuwajua vyema washindani hao wakubwa katika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi.

Mhe. Lissu amesema kuwa ushiriki wa midahalo kwa wagombea urais ni mojawapo ya kipimo muhimu kinachotumika kimataifa kujua uwezo wa wagombea urais na kwa hapa nchini, takriban wiki mbili tangu kuanza kwa mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu, Agosti 26, mwaka huu, haina shaka yoyote kuwa ushindani katika nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uko kati ya Mgombea wa Chadema na Mgombea wa CCM, ambapo amesisitiza wito huo kwa kuviomba vyombo vya habari vikubwa hususan vituo vya luninga, kuandaa mdahalo huo.

“Natoa rai kwa mgombea mwenzangu wa CCM, tukutane kwenye mdahalo. Ufanyike kwa lugha yoyote ile na uendeshwe na wataalam tutakaokubaliana. Ili tuwaeleze na tuhojiwe hadharani na kujibu hadharani mipango na maono yetu. Naamini mwenzagu ambaye ameshakuwa Rais kwa miaka mitano hatakuwa na hofu ya kushindana na mimi ambaye sijawahi kuwa Rais. Tukutane pamoja. Tuache haya mambo ya kuogopana na kuchengana. Nina imani hatakimbia mdahalo. Akiogopa tutahoji majigambo ya usomi wake,” amesema Mhe. Lissu.

Aidha, Mhe. Lissu amesema Serikali atakayoiunda chini ya chama CHADEMA, itaondoa mara moja masharti ya kibaguzi na utaratibu mbovu wa kisheria unaotumika katika mfumo wa sasa wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ambao umegeuka kuwa adha kubwa kwa wanafunzi na wazazi na badala yake, kanuni pekee itakayosimamia upatikanaji wa mikopo hiyo ni uhitaji wa mhusika.

Akisisitiza hoja hiyo, Mhe. Lissu amesema kuwa mfumo wa urejeshaji riba ya mikopo hiyo unaotumika sasa nao pia uko kinyume na utaratibu wa kisheria uliokuwa mwongozo kwa wanafunzi na wazazi kuingia makubaliano ya kukopeshwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini (HESLB), ambapo Serikali imeingiza utaratibu mwingine kuwataka wanufaika kulipa riba ya asilimia 15 badala ya asilimia 3 ya awali, akiahidi kuwa Serikali ya Chadema itaufutilia mbali kwa sababu unawafilisi kiuchumi wanufaikaji wa mikopo hiyo.

Akihutubia mkutano wa Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, uliohudhuriwa na maelfu ya wananchi wa Mji wa Iringa na viunga vyake, uliofanyika leo katika Uwanja wa Mwembetogwa, Mhe. Lissu amesema mfumo unaotumika sasa umewekewa utaratibu ambao unawaumiza na kuwabagua wanafunzi na wazazzi hata wenye uhitaji wa mikopo hiyo ili waweze kujielimisha elimu ya juu kwa kadri ya uwezo wao.

Aidha, Mhe. Lissu akizungumzia umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa watu wote bila kubagua hali wala hadhi ya mtu, amesema kuwa kila mmoja katika wakati usiotarajiwa anaweza kuhitaji msaada wa kuhifadhiwa iwe kwa matibabu, ulemavu usiotarajiwa, umri wa uzeeni, kupoteza ajira au uhitaji wowote ule, hivyo Serikali atakayoiunda, akichaguliwa Oktoba 28, mwaka huu, itaweka utaratibu utakaohakikisha kila Mtanzania anapata hifadhi kadri ya ya mahitaji, ikiwemo bima ya afya, badala ya sasa wanaohudumiwa walioko kwenye ajira rasmi pekee.

“Iringa ni mahali sahihi kabisa kuzungumzia agenda ya hali ya elimu yetu na hususan elimu ya juu. Kuna tatizo katika mfumo wetu wa utoaji elimu nchini. Mtakumbuka wakati ule nilipokuja wakati wa kutafuta udhamini nilizungumza hili. Tunapaswa kuubadili ili uweze kuwapatia watoto wetu maarifa na uwezo wa kufikiria kutatua matatizo yao na kuajiriwa mahali popote duniani.

Kwa sababu hilo nililisema wakati ule na mlinielewa, leo nataka nizungumzie hili la elimu ya juu na hususan elimu ya juu, chuo kikuu. Wale wa makamo yangu wanajua kuwa wakati wetu elimu tuliyosoma ililipwa na umma wa Watanzania. Katika zama za CCM wanaita ya kisasa, ili motto wako asome Chuo Kikuu lazima umlipie au akopeshwe na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, mikopo hiyo na utaratibu wa utoaji wake na urejeshaji wake, imegeuka kuwa adha kubwa mno kwa wazazi na wanafunzi wenyewe.

“Kumekuwa na masharti ya kibaguzi katika utoaji wa mikopo ya hiyo. Wanafunzi waliosoma shule za binafsi wamekuwa wakiambiwa hawastahili kupata mikopo. Wanafunzi wengine wengi wameshindwa kuendelea na masomo yao. Serikali ya Chadema, nitakayoiunda mkinichagua Oktoba 28, mwaka huu, itaweka utaratibu unaohakikisha kila mtoto anastahili kupata mkopo bila kujali alisoma wapi. Kanuni pekee itakayotuongoza ni, je anahitaji mkopo? Tutahakikisha pia wanufaikaji wote wanatendewa haki kwa kurejea kwenye sheria ya mwanzo iliyokuwa inaelekeza makato ya riba ya asilimia 3 badala ya sasa ambapo imefanywa kuwa asilimia 15 hali inayowafilisi kiuchumi,” amesema Mhe. Lissu.

Akitumia mkutano huo pia kuomba kura zake na kuwaombea kura wagombea ubunge na udiwani kwa tiketi ya Chadema katika Mkoa wa Iringa, Mhe. Lissu amezungumzia umuhimu wa hifadhi ya jamii kwa watu wote, ambapo amesema kuwa mfumo uliopo sasa pamoja na kuwatenga watu wengine wasiokuwa kwenye ajira rasmi, pia umeshindwa kuwahudumia hata wahusika baada ya kutumiwa vibaya kwa matumizi yasiyokuwa na tija kwa wachangiaji, ambapo amesema fedha nyingi zimefujwa kiasi cha mifuko hiyo kushindwa kujiendesha na hatimae kufilisika.

Ameongeza kuwa tatizo la hifadhi ya jamii si uwingi au uchache wake, bali ni matumizi mabaya ya rasilimali zake, hivyo ameahidi kuwa Serikali atakayoiunda baada ya kuchaguliwa mwezi Oktoba, itahakikisha utaratibu mpya wa hifadhi ya jamii unawahusisha watu wote kwa ajili ya maendeleo yao na kuhakikisha inaendeshwa katika namna inayozingatia matumizi sahihi yenye tija kwa wahusika ambao watakuwa na uhuru wa kuamua.

“Tunazungumzia mfumo wa hifadhi ya jamii utakaoweza kuwahudumia watu wote, wastaafu wetu, wazee, wasiojiweza, bima ya afya. Tutahakikisha kila asiyejiweza anatunzwa na hifadhi ya jamii. Sisi wote hapa tutazeeka, tunaweza kuwa walemavu, tunaweza kupoteza ajira, tutaugua, tutahitaji kuhifadhiwa. Shida hapa kwetu si wingi wa mifuko, bali mifuko hiyo imefujwa. Walipoifilisi wakaleta masuala ya fao la kujitoa na ile kanuni mpya ya kikotoo, maana mifuko hiyo haina fedha tena,” amesema Mhe. Lissu.

Mhe. Lissu amesema kuwa utekelezaji wa mipango hiyo utahitaji vyanzo vya uhakika vya fedha, ambapo ametaja mapato yatakayotokana na uuzaji wa gesi asilia, ambayo uendelezaji wake ulianza wakati wa Serikali ya awamu ya nne, ulioibainisha Tanzania kuwa mojawapo ya nchi zenye utajiri mkubwa wa rasilimali hiyo, kabla haujatelekezwa katika awamu ya tano, itakuwa ni mojawapo ya vyanzo vya fedha ili kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata elimu ya uhakika na Watanzania wote wanapewa haki ya hifadhi ya jamii.

Mhe. Lissu ametumia mikutano yake mitatu katika maeneo ya Migoli (Isimani), Ifunda (Kalenga) na Iringa mjini, kunadi agenda mbalimbali zilizomo katika Ilani ya Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, inayozungumzia masuala yote katika muktadha wa Uhuru, Haki na Maendeleo ya Watu.

Imetolewa na Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano – Chadema

Previous articleUganda and Tanzania Sign $3.5bn Oil Pipeline Deal
Next articleUN Imetahadharisha Tanzania Kuepuka Mazingira Ya Ukandamizaji Ambayo Yanaweza Kusababisha Madhara Makubwa