
Mgombea urais Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA), Mh. Tundu Lissu, amesema akishindwa kwa haki kwenye nafasi ya urais anayogombea kwenye uchaguzi mkuu, atakuwa wa kwanza kusema kuwa ameshindwa kwa haki.
Mh. Lissu ameendelea kusema, wakishinda lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania (NEC) ikawapora ushindi wao, atawaingiza wananchi barabarani kuteteta ushindi wao.

Amesema chama chake cha CHADEMA wakishinda uchaguzi huo, ni lazima Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) itangaze kwa heri au kwa shari.
Amesisitiza wanataka Uchaguzi wa amani, lakini hawatakuwa tayari kugeuza shavu la pili ili waumie zaidi. Ameyasema haya alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni za uchaguzi mkoani Tabora.

Uchaguzi wa mwaka huu umeleta ushindani mkubwa baina ya Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania, Mh. John Magufuli na Mh. Tundu Lissu. Wagombea hawa wawili wameweza kukusanyana maelfu ya wafuasi kila wanapofanya mikutano yao ya kampeni.

Uchaguzi mkuu wa Tanzania unatarajiwa kufanyika tarehe 28 Oktoba, 2020 na utachagua rais, wabunge na madiwani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.