Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. John Pombe Magufuli amefariki dunia siku ya leo Jumatato, tarehe 17/3/2021 wakati akipatiwa matibabu ya matatizo ya moyo katika hospitali ya Mzena jijini Dar Es Salaam, Tanzania.

Rais Magufuli ambaye ndio alikuwa anaanza muhula wake wa pili wa urais kwa miaka mingine mitano, aligua kwa siku chache na hatimaye mauti kumkuta.

Rais Magufuli atakumbukwa kwa kujizolea sifa nyingi kutoka sehemu mbalimbali duniani kutokana na zoezi lake la kupiga vita rushwa, huku akiwafukuza watendaji mbalimbali wa serikali waliozembea makazini kwa kushindwa kutimiza majukumu yao kwa staili ya kutumbua papo kwa hapo.

Mpaka kifo kinamkuta, alikuwa pia Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi ambacho ndio kinashikilia madaraka ya kuongoza Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Pamoja na serikali kutangaza kupitia Makamu wa Rais, Samia Suluhu, kwamba chanzo cha ugonjwa kilichosababisha mauti ya Rais Magufuli ni matatizo ya moyo, yaliyotokana na hitilafu ya kifaa cha “Pacemaker” ambacho alikuwa nacho moyoni kwa miaka 10. Wadadisi wengi na wadau mbalimbali wa kisiasa, wanadai kifo chake kitakuwa kimesababishwa na ugonjwa wa Covid-19 unaotokana na virusi vya Corona.

Wasaidizi wa karibu wa Rais Magufuli walifariki siku za karibuni kunakopelekea wengi kuuhusisha ugonjwa huo na kifo chache.

Picha inayoleta gumzo mitaani kutokana na wahusika wote kwenye picha hii kufariki katika kipindi kifupi. Kwenye picha anaonekana Balozi Augustine Mahiga akila kiapo alipoteuliwa Waziri wa Katiba na Sheria. Balozi Mahiga alifariki Mei 1, 2020. Aliyefuatia ni Balozi John Kijazi aliyefariki Februari 17, 2021 ambaye alikuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Mwingine ni Oswald Simon Majuva aliyekuwa msaidizi wa Rais aliyefariki Machi 12, 2021. Rais Magufuli naye amefariki Machi 17, 2021.

Pamoja na wasaidizi hao waliofariki kwa kipindi kifupi, pia kumekuwa na ongezeko kubwa la vifo vya wanasiasa, wafanyabiashara, wanasheria, maprofesa, na hata majaji mbalimbali ndani ya Tanzania.

Aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa serikali ya mapinduzi ya Zanzibar, Mh. Seif Sharrif Hamad, alifariki Februari 17, 2021 baada ya kuugua Covid-19.

Mwenyezi Mungu ampumzishe kwa amani Rais John Magufuli. Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa, Jina Lake Lihidimiwe.

Previous articleBREAKING NEWS: PRESIDENT MAGUFULI IS DEAD
Next articleMfahamu Samia Suluhu Hassan Rais Mtarajiwa wa Tanzania