
Baada ya siku kadhaa za maandamano ya vijana nchini Nigeria huku wakiongozwa na wasanii maarufu kushinikiza kuvunjwa kwa kilichokuwa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Wizi (Special Anti-Robbery Squad maarufu kama SARS), Mkuu wa Jeshi la Polisi wa Nigeria, Mohammed Adamu, ametangaza rasmi kuvunjwa kwa kikosi hiko.

SARS, ambacho kilikuwa kitengo maalumu chini ya jeshi la polisi la shirikisho la Nigeria toka mwaka 1992, kwa muda mrefu kimekuwa kikilaumiwa kwa unyanyasaji, ukamataji pasipo kufuata sheria, utesaji na hata mauaji.
Maandamano ya sasa yakichagizwa na wasanii wakubwa wa muziki nchini Nigeria kama Davido, Falz, na Runtown, yalizuka baada ya video moja kusambaa ikiwaonyesha askari wa SARS wakimpiga risasi hadi kumuua raia mmoja wa kiume katika jimbo la Delta ya Kusini.

Davido aliandika kwenye mtandao wa Twitter juu ya mkutano wake na IGP, Mohammed Adamu.
I am meeting with the inspector general of police tomorrow 10 am …. all my colleagues if u can get to Abuja 2moro before 10 am and follow me to the meeting ! It would mean a lot ❤️
— Davido (@davido) October 11, 2020
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria, alitoa amri ya kuvunjwa kwa kikosi hicho baada ya kukutana na Mkuu huyo wa jeshi la polisi la nchi hiyo.


Wakati hayo yakitokea nchini Nigeria, ambapo wasanii maarufu pamoja na vijana mbalimbali walipoamua kufanya maandamano dhidi ya serikali na jeshi la Polisi la nchi hiyo, nchini Tanzania hali ni tofauti kabisa kutokana na wasanii wote wakubwa kuwa bega kwa bega wakishirikiana na chama tawala kinachoongozwa na Mh. Rais John Magufuli.
Wasanii wengi wa Tanzania, kama Diamond Platnumz, Alikiba, Harmonize, na Nandy ambao hivi sasa wanazunguka sehemu mbalimbali za nchi kunadi sera za CCM na huku wakimpigia kampeni kwa kutoa burudani za bure kwa wananchi ili Rais Magufuli aweze kuchaguliwa tena kwa miaka mingine mitano.



Lipo pia kundi dogo la wasanii ambao wamekuwa wakiunga mkono vyama vya upinzani lakini idadi yao na umaarufu wao sio sawa na wale wanaounga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani nchini Tanzania utafanyika siku ya tarehe 28 Oktoba, 2020 ambapo Rais Magufuli ameomba tena ridhaa ya Watanzania kuendelea kuongoza kwa miaka mingine mitano. Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha CHADEMA kimemsimamisha Tundu Lissu kama mgombea wake.