Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright akifanya mazungumzo na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar Es Salaam.

Nilifika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza zaidi ya miaka 30 iliyopita kufanya kazi ya kujitolea kama daktari na uzoefu huo ulinifanya nijenge heshima na mapenzi ya kina na ya kudumu kwa Tanzania na Watanzania. Ilikuwa ni heshima kubwa sana katika maisha yangu, baada ya miaka mingi, kupewa fursa ya kurejea tena nchini humu kuhudumu kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania. Toka nilipowasili hapo mwezi Agosti, nimekuwa nikizungumza namna msaada wa Marekani unavyoboresha maisha ya Watanzania wa kawaida na jinsi ya  kukuza ushirikiano na biashara kutakavyoweza kuwanufaisha watu wetu.

Uhusiano kati ya Marekani na Tanzania unaturejesha nyuma hadi siku za mwanzo za uhuru ambapo urafiki kati ya Rais Kennedy na Mwalimu Nyerere uliweka misingi ya ushirikiano imara uliojengwa katika kuheshimiana na kuelewana, huku kiini cha uhusiano huo kikiwa ni  kuleta hali bora zaidi na ustawi wa watu wa nchi zote mbili.  Katika kusaidia kufikia lengo hilo, Marekani, katika mwaka 2020, itachangia zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 546 katika jitihada za maendeleo ya kiuchumi na kijamii za Tanzania. Aidha, katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 iliyopita Marekani imetoa msaada wa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 7.5 kwa Tanzania, sehemu kubwa ya msaada huo ukielekezwa katika kuboresha afya ya Watanzania. Aidha, kwa fahari kubwa,  Serikali ya Marekani inawekeza kwa watu wa Tanzania kwa kuwawezesha vijana wake wenye vipaji mbalimbali kushiriki katika programu za mabadilishano ikiwemo ile ya kuwajengea uwezo wa kiuongozi vijana wa Afrika (Young African Leaders Initiative –YALI). Hali kadhalika, sekta binafsi ya Marekani imewekeza pia nchini Tanzania, ikichangia kuongeza nafasi za ajira kwa Watanzania na kukuza ustawi kwa nchi zetu mbili.

Wakati huohuo,  nikiwa nahimiza umuhimu wa biashara na uwekezaji, nimekuwa pia nikipaza sauti kuelezea umuhimu wa haki za msingi za binadamu na michakato ya kidemokrasia – ikiwa ni pamoja na chaguzi huru na za haki – kama msingi muhimu sana wa maendeleo endelevu.

Kuhimiza kuwepo kwa chaguzi huru na za haki si kuingilia siasa za Tanzania, bali ni kusimamia na kulinda matamanio ya msingi ya watu wote, Wamarekani na hali kadhalika Watanzania: matamanio hayo ni kuona kuwa sauti zao zinasikika, hususan pale linapokuja suala la kuchagua ni nani awaongoze na kuwawakilisha.

Ningependa kuwa wazi kabisa kuhusu suala hili: Marekani haimuungi mkono mgombea au chama chochote cha siasa katika kampeni hizi za uchaguzi. Cha msingi kwa Marekani katika uchaguzi huu ni kwamba unakuwa huru, wa haki na wa kuaminika na kwamba matokeo yake yataakisi maamuzi ya watu wa Tanzania kama walivyoyaeleza katika sanduku la kura. Hiki ndicho kielelezo halisi cha demokrasia.

Lakini kwa masikitiko makubwa, nimeona na kusikia taarifa za serikali na vyombo vya usalama kuingilia na kukwaza uwezo wa wagombea kufanya kampeni zao kwa uhuru. Kwa kadri tunavyoisogelea siku ya uchaguzi, ndivyo kasi na ukubwa wa vikwazo hivyo inavyoongezeka. Tumeshuhudia vurugu za kisiasa, kuminywa kwa vyombo vya habari na mchakato wa uteuzi wa wagombea ambao hata kwa muonekano wake tu, unatoa upendeleo wa wazi kwa chama tawala. Tayari tumeanza pia kusikia taarifa za maafisa kukwaza uwezo wa mawakala wa vyama kufanya kazi zao. Ukiyaangalia kwa pamoja, mambo haya yote yanajenga taswira ya mchakato wa uchaguzi unaoonekana kutokuweka uwanja sawa kwa wahusika wote.

Kwa bahati nzuri, bado kuna muda wa kuweza kuhakikisha kuwa uchaguzi wa Oktoba 28 unakuwa huru, wa haki na wenye uwazi kwa kadri inavyowezekana. Uwazi huleta kuaminika na kuaminiwa.  Njia mojawapo ya kuhakikisha mchakato wa uchaguzi wenye uwazi ni kuruhusu waangalizi huru kushuhudia uchaguzi huo na kuwapa uhuru wa kueleza kile walichokishuhudia. Maafisa wa uchaguzi wanaweza kupiga hatua kubwa ya kurejesha imani ya watu kwa mchakato wa uchaguzi kwa kuhakikisha kuwa matokeo katika vituo vya kupigia kura yanawekwa wazi kwa umma, mawakala wote wa vyama wanaapishwa na katika siku ya uchaguzi wanaruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia na kuhesabia kura nchini kote pamoja na kupatiwa nakala za majumuisho ya kura (tallying sheets) mwishoni mwa zoezi la kuhesabu kura.  Kama alivyosema Jaji wa Mahakama Kuu ya Marekani, Louis Brandeis, “mwanga wa jua ni dawa nzuri zaidi ya kuua vimelea vya maradhi (sunlight is the best disinfectant”). Kwa maneno mengine, uwazi wa serikali unaweza kuhakikisha kuwa mchakato wa uchaguzi unakuwa wa kuaminika.  Nchini Marekani, tuna utamaduni wa muda mrefu wa kuwaalika waangalizi wa kimataifa wa uchaguzi kushuhudia uchaguzi wetu, na tunawakaribisha tena mwaka huu.

Wasiwasi wangu ni kuwa, iwapo maafisa wa uchaguzi hawatachukua hatua nilizozieleza hapo juu, demokrasia ya Tanzania itapoteza hali ya kuaminika katika macho ya jumuiya ya kimataifa. Muhimu zaidi, mgombea atakayetangazwa mshindi atakosa uhalali mbele ya macho ya Watanzania wenyewe.

Haya ni maoni ya balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald J. Wright.

Previous articleRuby – Yako Wapi Mapenzi
Next articleAfrica’s Week in Pictures: 16 – 22 October 2020