Rais John Pombe Magufuli, amemtumbua Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi, na Teknolojia, Dkt. Ave Maria Semakafu kutokana na kutangaza kwa kufutwa kwa mtaala wa ualimu wa ngazi ya cheti. Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Ndugu Gerson Msigwa, imesema Rais Magufuli ametengua utenzi wa Naibu Katibu Mkuu huyo kuanzia tarehe 05 Oktoba, 2020.
Kutumbuliwa kwake kumekuja siku moja baada ya Rais Magufuli kupiga simu kwenye kongamano la Chama Cha Walimu Tanzania kukanusha kufutwa kwa Ualimu Ngazi ya Cheti.
Tukio hili la kutumbuliwa kwa naibu katibu mkuu huyo limewashangaza wananchi wengi kutokana na kuamini kwamba, maamuzi makubwa kama hayo yanayofanywa na wizara au viongozi wakuu wa wizara lazima yapate baraka za Rais au Ofisi ya Rais.
Taarifa ya kufutwa kwa mafunzo iliyotolewa na wizara ya elimu kupitia kwa Dkt. Semakafu inaonyesha halikuwa ni jambo alilojiamulia peke yake, basi na maamuzi yaliyopitiwa na viongozi wote wizarani na hata Ikulu.
Na uchunguzi zaidi uliofanywa na Bongo Radio, umeonyesha pia hata ilani ya Chama Cha Mapinduzi inajumuisha muongozo wa kufuta mafunzo hayo ya ualimu ngazi ya cheti.