Timu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Lakers kutoka jijini Los Angeles, California, imechukua ubingwa wa NBA kwa mwaka 2020. Timu hiyo iliyokuwa ikiongozwa na mchezaji wao maarufu Lebron James, imechukua ubingwa huko kwa kuwafunga timu ya Miami Heat, kutoka jiji la Miami, Florida, kwa pointi 106-93.

Los Angeles Lakers’ LeBron James (23) akifurahi na wachezaji wenzake baada ya kutwaa ubingwa wa NBA kwa timu yake ya Lakers kuifunga Miami Heat kwa pointi 106-93 kwenye mchezo wa 6 wa fainali hizo zilizofanyika kwenye mji wa Lake Buena Vista, Florida siku ya Jumapili, Oct. 11, 2020. (AP Photo/Mark J. Terrill)

Ligi hiyo iliyokuwa ya aina yake kwa mwaka 2019-2020, ilichukua kipindi cha miezi mitatu mpaka kumalizika kutokana na kusimama kwa muda mrefu kwa sababu ya kuepuka maambukizi ya virusi vya corona. Timu zilizoshiriki ziliwekwa kwenye eneo maalumu ambapo wachezaji, makocha na hata waandishi wa habari hawakuruhusiwa kutoka eneo hilo.

Kufanikisha ligi hiyo kwa usalama bila ya maambukizi ya coronavirus na hatimaye ugonjwa wa covid-19, uongozi wa ligi hiyo ya NBA iliamua kuwapima corona kila siku, wachezaji, makocha na wahusika wengine wote waliokuwa na ushiriki kwenye ligi hiyo. Umakini umeonekana kwani mpaka ligi hiyo ilipoisha na bingwa kutangazwa hakuna hata mtu mmoja alieambukizwa corona.

Timu hiyo ya Los Angeles Lakers ilipatwa na msiba mkubwa tarehe 26 January, 2020, kutokana na kifo cha mchezaji wao zamani maarufu, Kobe Bryant. Mchezaji huyo alifariki kutokana na ajali ya helicopter iliyotokea katika kitongoji cha Calabasas, jijini Los Angeles, California. Kobe, alifariki kwenye ajali hiyo pamoja na mtoto wake wa 13 anayeitwa Gianna, na watu wengine saba waliokuwa wakisafiri nao kwenda kwenye kituo cha michezo cha Mamba Sports Academy katika mji wa Thousand Oaks.

Eneo la ajali ya helicopter iliyokuwa imembeba Kobe Bryant, mtoto wake Gianna, pamoja na watu wengine saba ambao wote walifariki dunia.

Ligi hiyo ya mwaka huu pia ilileta umoja miongoni mwa wachezaji wote wa NBA kupinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani. Kampeni hiyo ililenga unyanyasaji na udhalilishaji wa polisi dhidi ya raia weusi wa nchi hiyo. Huku wachezaji wakiongozwa na Lebron James, ligi hiyo ilichukua hatua mbalimbali ikiwemo kusitisha michezo, baada ya timu ya Milwaukee Bucks kugomea mchezo wake kutokana na raia mweusi anayeitwa Jacob Blake kupigwa risasi na polisi mjini Kenosha, Wisconsin. Jezi za timu za NBA ziliwekwa lebo za Black Lives Matter.

Huu utakuwa ni utakuwa ni ubingwa wa nne kwa Lebron James ambao ameupata kwa timu tatu tofauti ambazo ni Miami Heat, Cleveland Cavaliers na sasa akiwa na Los Angeles Lakers. Ubingwa huu pia unaifanya timu ya Los Angeles Lakers kuwa imechukua ubingwa wa NBA kwa mara 17 ikiwa na idadi sawa na timu ya Boston Celtics.

Previous articleRapper Tory Lanez Charged in Shooting of Megan Thee Stallion
Next articleFire Breaks Out on Africa’s Tallest Mountain – Kilimanjaro