Unapozungumzia hifadhi 16 za taifa, Mbuga ya Saadani siyo maarufu masikioni mwa Watanzania wengi.

Pengine hii inatokana na kupandishwa hadhi miaka ya hivi karibuni. Pia inawezekana ni kwa sababu ya kukosa matangazo ya kutosha ndani na nje ya nchi.

Licha ya kutofahamika kwake, Saadani ni hifadhi ya kipekee yenye vivutio vizuri vya kitalii vinavyoweza kulitangaza taifa na kuongeza pato lake. Hifadhi hii ina rekodi ya aina yake kwa kuwa na vitu ambavyo hazipatikani katika mbuga nyingine.

Tofauti na hifadhi nyingine, Saadani pia inahifadhi mali kale na wanyama wengine wa majini. Wageni mbalimbali wa ndani na nje ya nchi hutembelea eneo hili ili kujionea maliasili zilizopo sambamba na mandhari nzuri ya hifadhi yenyewe.

Mbali na kuwepo kwa wanyamapori tuliowazoea hasa wale watano maarufu, simba, tembo, nyati, twiga na faru, hifadhi hii inayopakana na Bahari ya Hindi, ina fukwe nzuri, jambo linaloifanya iwe ya kuvutia.

Hifadhi hii inapokea watalii wasiopungua 500 kwa mwaka kutoka nje ya nchi, sawa na asilimia chini ya moja ya watalii wanaotembelea Hifadhi ya Serengeti. Pengine idadi hii ndogo inatokana na kutofahamika kwa Saadani, pia mwamko mdogo wa utalii wa ndani.

Asili ya Hifadhi ya Saadani

Hifadhi ya Saadani iliyo chini ya Mamlaka za Hifadhi za Taifa (Tanapa) ilianzishwa mwaka 1962 ikiwa ni pori la akiba. Baadaye mwaka 2005, ilipandishwa hadhi rasmi na kuwa hifadhi ya taifa.

Mwongoza watalii katika hifadhi hiyo, Akwilini Swai anasema jina la hifadhi hiyo limebeba jina la Kijiji cha Saadani ambalo kilitokana na jina alilopewa mwarabu aliyekuwa anaishi na kufanya biashara katika eneo hilo lililokuwa likijulikana kama Utondwe.

Anasema mwarabu huyo alikuwa mtu pekee katika Kijiji cha Utondwe aliyekuwa akimiliki saa ya ukutani. Watu walikuwa wanakwenda kwake kuangalia muda kwa sababu aliiweka saa hiyo nje.

Swai anasema baadaye mwarabu huyo aliamua kuiweka ndani saa hiyo ili kuepuka usumbufu aliokuwa anaupata kutoka kwa watu waliokuwa wanakwenda kwake.

Watu walipokwenda na kumuuliza; saa ngapi?, alikuwa akiwajibu: ‘saa ndani’ akimaanisha kuwa saa iko ndani. Baadaye alipokuwa akijibu mara kwa mara akawa anakosea na kusema ‘saa dani’ akiwa na maana ile ile kuwa saa iko ndani.

“Mtu alikuwa akiulizwa unakwenda wapi alijibu saadani, basi eneo hili likafahamika zaidi kama Saadani, kutokana na makosa ya matamshi ya mwarabu wakati ule,” anafafanua Swai.

Hifadhi hii inayopatikana katika pwani ya maeneo ya Pangani, Bagamoyo na Handeni, ilikuwa pia eneo la uwindaji. Wanakijiji walifanya shughuli zao za uwindaji ili kuendesha maisha yao.

Vivutio vya utalii

Saadani ndiyo hifadhi pekee barani Afrika inayopakana na bahari. Ukanda wote wa pwani kuanzia pwani ya Bagamoyo hadi Handeni ni eneo la hifadhi hii na watalii wanapata nafasi ya kubarizi katika fukwe zake.

Mhifadhi utalii wa Hifadhi ya Taifa ya Saadani (Sanapa), Rukia Malya anasema Saadani inakutanisha sehemu ya hifadhi na Bahari ya Hindi. Wanyama na ndege mbalimbali hupenda pia kucheza katika baadhi ya maeneo ya fukwe hizo.

Anasema kuwepo kwa bahari kunaiongezea mvuto hifadhi hiyo nakuifanya kuwa ya kipekee katika ukanda wa Afrika. Malya anabainisha kuwa kuwepo kwa bahari kumewezesha pia kuwa na vivutio vingine hasa viumbe wa baharini.

Mbali na kuwa na fukwe nzuri, anasema hifadhi hiyo ina mazalia ya kasa wa kijani. Kasa hawa hutoka baharini kwenda nchi kavu kutaga mayai kisha wanayafukia. Baada ya vifaranga kutotolewa, wanarudi tena katika eneo lili lile kutaga mayai mengine.

“Kasa wanaopatikana sehemu nyingine ni wa kawaida. Hawa wa kwetu ni wa kijani na wana tabia tofauti na wale wanaopatikana sehemu nyingine,” anasema Malya na kuhimiza watu kutembelea eneo hilo ili kujionea.

Baadhi ya wanyamapori wanaopatikana katika hifadhi hiyo, anawataja kuwa ni twiga, tembo, simba, nyati, swala, kiboko na mamba. Pia kuna zaidi ya aina 200 za ndege wakiwemo, wanaohama.

Aidha, anaeleza kuwepo kwa mali kale zenye kuakisi mila na desturi za wenyeji wa mkoa wa Pwani na maeneo mazuri yenye mabaki ya kihistoria. Misitu ya mikoko na ile ya ukanda wa pwani, pia vinaiongezea mvuto hifadhi hiyo.

Ujangili katika hifadhi

Malya anafafanua kuwa zamani ujangili ulikithiri kwenye hifadhi hiyo. Kwa mujibu wa Swai, mnyama aliyeuawa sana wakati huo alikuwa faru, jambo lililosababisha atoweke kabisa.

Anasema wanajitahidi kuilinda hifadhi hiyo dhidi ya majangili wanaorudisha nyuma jitihada za Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika kuhifadhi maliasili za wanyama kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

“Tuna wanyama wote wakubwa katika hifadhi hii isipokuwa faru tu. Hii imetokana na vitendo vya kijangili dhidi ya mnyama huyo. Wananchi watambue kuwa vitendo vya ujangili hujuma kwa taifa vina madhara makubwa,” anasema mhifadhi huyo.

Hata hivyo, anasema sasa hali ni shwari, kwa kuwa baadhi ya wanyama waliongezwa kutoka hifadhi nyingine za Mikumi na Selous na sasa wanazaliana na kuongeza idadi ya wanyama wanaopatikana katika hifadhi hiyo.

Watanzania na utalii

Ofisa uhusiano mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa), Catherine Mbena anasema Watanzania bado hawana mwamko mkubwa wa kutembelea hifadhi japo gharama yake ni ndogo.

Anasema watu wengi wanalalamikia gharama za kuingilia katika hifadhi hizo, japo wakiulizwa wataje ni kiasi gani wanashindwa kutoa majibu.

“Tunajitahidi kutoa elimu kwa wananchi na kutangaza vivutio tulivyonavyo. Lakini bado Watanzania hawatembelei hifadhi zetu, sijui tatizo ni nini,” anahoji Mbena na kuongeza kuwa ni muhimu kutembelea hifadhi kwani kuna mambo mengi ya kujifunza na kuburudika.

Anazitaja gharama za kuingilia katika hifadhi za taifa kuwa ni Sh5000 kwa Watanzania wenye umri zaidi ya miaka 16, Dola 30 za Marekani kwa raia kutoka nje ya Afrika Mashariki na Dola 15 kwa raia wengine wa Afrika Mashariki.

Kwa watoto kuanzia umri wa miaka mitano hadi 16, anasema Watanzania wanalipa Sh2000, ilhali wageni nje ya Afrika Mashariki ni Dola za Marekani 10 na wale wa Afrika Mashariki ni Dola tano na watoto chini ya miaka mitano wote ni bure.

Last News

Previous articleVanessa Mdee Azungumzia Fitna Katika Muziki Tanzania
Next articleLady Jaydee