Kampuni ya inayotoa huduma za usafiri ya Uber, imeamua kusitisha kwa muda kutoa huduma zake nchini Tanzania kulingana na taarifa iliyosambazwa na Uber Tanzania kwa njia ya mtandao.
Kampuni hiyo imedai kuwa imeamua kufikia uamuzi huo kutokana na kanuni mbalimbali za usimamizi wa sekta ya usafiri kuwa na mazingira ambayo si rafiki na kuleta changamoto kubwa katika uendeshaji wa biashara yao.
Taarifa hiyo imedai, huduma za usafiri za UberX, UberX Saver na UberXL zitasimamishwa kwa muda mpaka muafaka utakapofikiwa.
Uber Tanzania imekuwa ikitoa nchini Tanzania kwa miaka sita sasa, na umaarufu wake umezidi kuongezeka kila mwaka kutokana na kuongezeka kwa mahitaji makubwa ya usafiri.
Jitihada za kuwasiliana na wahusika kutoka ofisi za Uber ziligonga mwamba. Uber itasimamisha shughuli zake siku ya Alhamisi tarehe 14, April.