Na Shufaa Lyimo

RAISI wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa bilioni 1.5 kwa ajili ya kuuinua mfuko wa wasanii ukiachilia bilioni 1.5 aliyoitoa hapo awali.

Hayo yalisemwa jana, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Omary Mohamed Mchengerwa, wakati alipokuwa anawaaga wasanii wa tamthilia ya Huba inayorushwa kwenye kituo cha televisheni cha DSTV, muda mfupi kabla hawajapanda pipa kuelekea nchini Dubai walipoalikwa na wadau wa tamthilia hiyo ikiwemo kwenda kushuti kazi nyingine.

“Ninatambua mmefanya kazi mkubwa kwa kutumia nguvu zenu binafsi serikali inatambua mchango wenu ninaomba mkautangaze zaidi utamaduni wetu, alisema Mchengerwa.

Waziri huyo alisema Rais ametambua thamani yao hivyo ameahidi kuuchangia mfuko huo kila mwaka.

Alisema Serikali itakuwa nao bega kwa bega kuhakikisha wanafika mbali zaidi ikiwemo kuwapa mikopo isiyokuwa na riba, pamoja na kufungua kituo cha redio na televisheni zitakazokuwa zinarusha kazi zao.

Aliwataka kwenda kuitagaza vizuri nchi yetu kupitia kazi yao hiyo na kuwatakia kila la heri katika safari yao.

Alisema watahakikisha wanakuwa nao bega kwa bega ili wazidi kusonga mbele kupitia vipaji vyao.

Naye rais wa Bodi ya Filamu Tanzania Elia Mjata alisema anaishukuru serikali kwa kuamua kuwa nao bega kwa bega  kuhakikisha wanafikia malengo.

Alisema tamthilia hiyo imefanya vizuri Afrika Mashariki na kudai watazidi kuinua vipaji.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Huba Aziz Mohamed alisema tamthilia hiyo imefanya vizuri kuanzia mwaka 2016-2022 ambapo imeweza kusaidia vijana kupata ajira.

“Tamthilia hii imefanya vizuri na vile vile vijana wengi wamepata ajira tunaishukuru serikali kwa jinsi walivyokuwa karibu na sisi tunaahidi kuiwakilisha nchi yetu vizuri, alisema Mohamed.

Naye Beny Kinyaiya ambaye alizungumza kwa niaba ya wasanii wenzake alisema tamthilia hiyo imeweza kufanya vizuri na yenye ubora Afrika Mashariki licha ya kuwa na changamoto za hapa na pale.

“Kila kazi ina  changamoto zake lakini pia tunashukuru kwa mafanikio tuliyoyapata ikiwemo hili la kualikwa na watazamaji nchini Dubai tutakwenda kuutangaza vizuri utamaduni wetu, alisema Beny.

Previous articleForbes’ Top 10 Highest-Paid Entertainers In 2022
Next articleMwenyekiti Wa Simba Afurahishwa Na Uwezo Wa Timu Yake