Serikali ya Urusi imeanza kutumia makombora ya kivita ya Kinzhal (Dagger) kuharibu ghala kubwa la silaha katika eneo la Ivano-Frankivsk magharibi mwa Ukraine.

Shirika la habari la Interfax la Urusi lilisema kuwa ni mara ya kwanza kwa kupeleka makombora hayo ya Kinzhal yenye nguvu nyingi tangu ilipotuma wanajeshi wake nchini Ukraine mnamo Februari 24.

Msemaji wa wizara ya ulinzi Igor Konashenkov aliambia mkutano mfupi kwamba bohari ya chini ya ardhi iliyopigwa na mfumo wa Kinzhal siku ya Ijumaa ilikuwa na makombora ya Kiukreni na risasi za ndege, kulingana na rekodi ya mkutano huo ulioshirikiwa na mashirika ya habari ya Urusi.
Msemaji wa ya jeshi la anga la Ukraine alithibitisha shambulizi la kombora la Russia katika eneo la Delyatyn katika mkoa wa Ivano-Frankivsk siku ya Ijumaa, bila kutoa maelezo zaidi.

Urusi inajivunia silaha zake za hali ya juu, na Rais Vladimir Putin alisema mnamo Desemba kwamba Urusi ndiyo inayoongoza ulimwenguni katika makombora ya hypersonic, ambayo kasi yake, na teknolojia iliyotengezwa hufanya iwe ngumu kuyafuatilia na kuyatungua.

Makombora ya Kinzhal ni sehemu ya safu ya silaha za Urusi zilizozinduliwa mnamo 2018.

Konashenkov aliongeza siku ya Jumamosi kwamba vikosi vya Urusi pia vimeharibu vituo vya redio vya kijeshi na upelelezi karibu na mji wa bandari wa Odessa wa Ukraine kwa kutumia mfumo wa makombora wa pwani wa Bastion.

Moscow inarejelea hatua zake nchini Ukraine kama “operesheni maalum” ya kudhoofisha uwezo wa kijeshi wa jirani yake wa kusini na kuwaondoa watu ambao inawaita wazalendo hatari.

Vikosi vya Ukraine vimezidisha upinzani mkali na nchi za Magharibi zimeiwekea Urusi vikwazo vikali katika juhudi za kuilazimisha kuondoa majeshi yake.

Previous articleKusah – I wish
Next articleNatacha – LAMOTO