Huenda akizungumza unaweza usimwelewe, lakini Diamond Platnumz aliamua kufikiri nje ya boksi na kufanikiwa kufanya kile alichokuwa akikikusudia, leo hii tayari makumi ya wasanii wameanza kutembea katika nyayo zake.
Kwa mujibu wa staa huyu ambaye alifanya mahojiano ya ana kwa ana nyumbani kwake Sinza jijini Dar es Salaam, anasema lilikuwa ni wazo lake tangu mwaka 2009 alipoingia rasmi katika muziki kwa kuweka nadhiri kwamba lazima ahakikishe anaitangaza nchi yake kupitia sanaa.
Anasema ilikuwa safari ndefu yenye milima na mabonde, lakini amefanikiwa kufikia hatua za mwanzo na anaamini bidii ikiongezwa kwake na wasanii wengine, muziki huo utafika mbali.
“Muziki wa Tanzania kwa sasa unaenda kasi mno, ukiangalia msanii Shetta wimbo wake wa ‘Kerewa’ unapigwa karibu redio za Fm sita hivi tunavyoongea wiki hii, wimbo wake umeshika nafasi ya tatu kwenye Beat Fm ya jijini Lagos, zamani kibongobongo suala kama hili lilikuwa ndoto na halikuwezekana kabisa.”
Diamond anasema mitandao ya kijamii imechangia kukua kwa soko lao, lakini jitihada binafsi za wao wenyewe zimesaidia.
“Ukiangalia katika vyombo vya habari hasa mitandao namna watu wanavyojitangaza, video zinavyofanyika ni tofauti na zamani. Tulikuwa tunafanya muziki lakini tulikuwa hatujitangazi, sasa hivi msanii akitoa singo anatengeneza kava, matangazo, watu wanafanya muziki kama biashara, wanapanda jukwaani na madansa yaani nidhamu ipo katika muziki tofauti na zamani,”.
Hata hivyo, Diamond anasema anakumbana na changamoto nyingi hivi sasa katika maandalizi ya kazi zake kwani ana soko kubwa la ndani lakini pia soko pana la nje ambako analazimika kuwalisha mashabiki wake wapya.
“Mwenyezi Mungu kanijalia kuna mashabiki wananikubali na wananiamini ndani na nje ya nchi, changamoto ninayoipata kwa sasa ni kuhusu mashairi ya kazi zangu, nitatengeneza vipi wimbo ambao nje utaeleweka?” anahoji na kuongeza:
“Soko la Tanzania linachanganya, watu wanataka niimbe mtu kaachwa lakini mwenyewe naangalia hivi wimbo kama huu nje utakubalika? Yaani hicho ndiyo kitu kinachokuwa kinanivuruga akili yangu kwa hiyo inabidi huku nifanye wimbo wake na nje wake ndiyo maana hata ukiangalia katika wimbo wa ‘Bum Bum’ na ‘Mdogo Mdogo’ kuna vionjo tofauti,” anasema.
Licha ya ugumu wa kazi aliyonayo, anasema bado mapromota wamekuwa wagumu kuelewa na kurekebisha malipo ya wasanii, tatizo linalosababisha wengi kukata tamaa.
“Ningependa tukimbizane katika soko la kimataifa, lakini tatizo wasanii walio wengi na wenye uwezo wanalipwa malipo kiduchu yasiyolingana na kazi zao, wataweza vipi kufanya kazi zenye viwango kama ninavyofanya mimi?”
“Tatizo lipo kwa hawa mapromota, mtu hataki kukubali kwamba kuna kitu kimebadilika, kukubali kwamba wasanii nao wapo katika soko na inatakiwa muziki ubadilike, mapromota wakubali kwamba tunataka haya yarekebishwe ili muziki ubadilike malipo ya shoo yapande wasanii bado wananyonywa, lakini mimi sikubali hata siku moja ndiyo maana nimejitengenezea jina langu kwenye biashara,” anasema Diamond.
Muziki kwangu ni biashara
Anasema licha ya mashabiki wengi kupenda nyimbo zake, kuna siri ambayo imejificha. Diamond anaifichua siri hii na kuweka wazi kwamba muziki kwake anaufanya kama biashara na si fani au kipaji.
“Muziki siyo bahati nasibu ni biashara, ni lazima uingize hela yako nyingi kufanya muziki kama mfanyabiashara anavyoingiza fedha yake, ni lazima utoe fedha yako nyingi ili ufanye biashara ya muziki na hivi ndivyo ninavyoenda. Kuna mbinu za kufanya na si kwamba muziki wetu ni mbaya hapana, kwa nchi yoyote ukishajua mbinu kwa wakati ulipo ni kitu gani kinatakiwa unaweza kufanya.”
Anasema kwa kutambua hilo, amejikita kutengeneza zaidi nyimbo maarufu zaidi badala ya muziki mzuri ambao kwa uzoefu wake wasanii wanaoimba muziki mzuri bado hawajapata mafanikio, lakini tatizo liko wapi, walaji wanataka nyimbo maarufu na nyingi hazina ujumbe makini.
“Kuna nyimbo nzuri na maarufu ‘hit song’, kuna wasanii wengi Tanzania wanaimba nyimbo nzuri lakini nyimbo zao hazipigwi. Unajua mfano Muziki Gani, Mdogo Mdogo, hizi zote ni ‘hit song’ lakini si nyimbo nzuri. Nenda Kamwambie, Kesho, Ukimwona hizi zote ni nyimbo ambazo niliimba nzuri. Kuna wasanii ambao wanaimba nyimbo nzuri, kama Ben Pol, Barnabas na wengineo, lakini soko letu linataka nyimbo maarufu,” anasema.
Hata hivyo, anasema ili ufanye biashara ya muziki, ni lazima uwe umewekeza katika video nzuri na iliyotengenezwa na waongozaji wakubwa wenye uwezo na vifaa makini.
“Muziki sasa umehamia kwenye video, hiki ni kitu cha pekee cha kukubali, audio peke yake wimbo wako kupendwa ni ngumu kwa sababu hata nyimbo nzuri kutoka nje, zinazopigwa Tanzania hatukuzijua kupitia audio ilikuwa ni video hata Nigeria tulianza kuziona video za kina P Square enzi zile,” anasema Diamond.
Bado natafuta madansa wa kike
Licha ya kuonekana na madansa wa kike katika jukwaa la Fiesta 2014 Mwanza, Diamond anasema hajabahatika kumpata dansa wa kike mwenye vigezo anavyovitaka.
“Sina madansa wa kike pale wawili ni wa Vanessa naweza sema wote si wangu, zamani nilikuwa na madansa wa kike, lakini kwa sasa Tanzania tuna upungufu kwenye muziki wa Bongo Fleva na muziki wa bendi kuna madansa ambao wamebobea kucheza muziki wa dansi pekee. Nilitamani kuwa na madansa wa kike zamani lakini ilishindikana maana kuwapata ni ngumu sana,” anasema na kuongeza:
“Mpaka sasa bado natafuta madansa wa kike sijawapata, nahitaji dansa wa kike ambaye anajua, awe anajiamini afuatilie madansa wa nje wanachezaje, awe na unyamwezi kidogo ni ngumu sana, awe mbunifu afuatilie muziki wa nje na vitu kama hivyo. Kwa hiyo nikatamani nifanyaje nikaamua kuazima madansa wa watu nifanye nao shoo,” anasema.
Akiwazungumzia madansa wake wa kiume ambao ni sita, Diamond anasema ni madansa wanaolipwa pesa ndefu ukilinganisha na madansa wote Afrika Mashariki.
Siwezi kusema nawalipa kiasi gani itakuwa kama nawavua nguo, lakini hakuna madansa wanaolipwa vizuri kama wangu Afrika Mashariki, ikiwa bei inaongezeka na mimi nawaongeza katika malipo yao. Wako sita kwa kweli nimetoka nao mbali tangu ‘Kamwambie’ mwaka 2009, nimekua nao kifikra, kiumri na kiakili na kuona kwamba hawa ni mzigo wangu mimi na wanafanya kazi pamoja na mimi, wale ni mafanikio yangu wana msaada mkubwa sana pengine nisingekuwa hapa bila wao,” anasema.
Hata hivyo, anaweka wazi kwamba linapofika suala la shoo za nje, huwa inategemea ni wapi kwani shoo zingine hairuhusiwi kwenda na madansa wote hivyo huwa anawabadilisha kwa zamu.
Unafiki upo muziki wa Bongo
“Naomba wananchi walitambue hili, muziki siyo fani ni biashara, wafanyabiashara wawili hawawezi kupendana lazima kutakuwa na unafiki ndani yake, kama wewe unafanya biashara ukampenda mwenzako hata mimi nitakuona mpuuzi.”
“Cha muhimu ni kusiwe na moyo ule wa chuki kumchukia mwenzako, lazima uweke moyo wa kwamba mwenzangu akipiga hatua na mimi nifikirie nifanye nini ili biashara yangu niiboreshe, siyo kuweka chuki hiyo haiwezi kuwa biashara. Watanzania wengi wanaamini kuwa ili upige hatua lazima amshushe mwenzie siyo kweli hauwezi kupanda juu kwa kumshusha mwenzako, lazima mtashuka wote au wewe utaonekana huna akili. Hata kampuni za simu zinashindana,” anasema.