Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia Na Maendeleo (CHADEMA) ambaye pia ni aliyekuwa Kiongozi wa Kambi Ya Upinzani Bungeni (KUB), Freeman Mbowe, ametangazwa kuwa ameshindwa kwenye nafasi yake ya ubunge kuliwakilisha jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro.
Mgombea kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM), Saashisha Mafue, ametangazwa mshindi kwa kupata kura 89,786 dhidi ya kura 27,684 alizopata Mbowe. Matokea hayo ambayo yamewashangaza wengi kutokana na mgombea huyo wa CCM kutokuwa anajulikana na wengi katika siasa za Tanzania.
Freeman Mbowe ambaye kwa kipindi kirefu amekuwa mwenyekiti wa CHADEMA, amekuwa ni kiungo kikubwa cha vyama mbalimbali vya upinzania nchini Tanzania.
Hadi tunakwenda mitamboni, matokeo mengine ya majimbo mbalimbali yalikuwa yanaaza kutangazwa, lakini inaonekana CCM itatangazwa mshindi kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Vyama mbalimbali vya upinzani vimedai uchaguzi huo uligubikwa na ubadhirifu mkubwa na hiyo ilitokana na kukuta wingi wa kura ambazo zilishapigwa kwa wagombea wa CCM.