Msanii wa Bongo Flava Amini Mwinyimkuu,maarufu kama “Amini” amevunja ukimya kwa kurudi tena katika muziki baada ya kimya cha muda mrefu.
Akizungumza na Bongo Radio, msanii huyo alieleza kuwa ukimya wake ulitokana na mambo mengi yaliyomkabili katika maisha, ambapo ilibidi ayatafutie ufumbuzi, mbali na kutoweka wazi yaliyomsibu na kusababisha kuwa kimya kimuziki. Amini alieleza kuwa kimya kingi kinamshindo na sasa amekuja kikamilifu kuendeleza safari yake ya kimuziki aliyoianza muda mrefu.
Aliongeza kwa kusema kwamba, hivi sasa ameachia ngoma mpya kabisa inayokwenda kwa jina la “Tujidai”, ngoma iliyofanyika katika studio ya State Muzic chini ya usimamizi wa mtayarishaji Geof Master.
Bongo Flava Video: Amini – Tujidai
Amin anaeleza kwamba, ngoma hiyo inafanya vizuri sana kwa sasa katika vituo mbalimbali vya habari lakini pia katika mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube.
Akitoa mtazamo wake kuhusu muelekeo wa tasnia ya muziki tanzania, alieleza kwamba tasnia ya muziki inazidi kufanya vema zaidi, kwani kwa sasa idadi ya wanamuziki inazidi kuongezeka na sanaa imekua ajira kwa kuongeza kipato miongoni mwa wasanii.
Amini anakana vikali taarifa zilizozagaa kuhusu kumuandikia msanii mwenzake (Beca Tittle) nyimbo iliyoitwa “Huyu Demu” ngoma ambayo waliifanya wote. Aliongeza kwa kusema kwamba, ngoma hiyo ni ya Beca Tittle, na yeye ameshirikishwa tu, hivyo sio kweli kwamba yeye ndio alieandika mashairi ya ngoma hiyo.
Aliendelea kusema kwamba, ushirikiano ni kitu muhimu sana kwa wasanii. Wasanii wanapaswa kushirikiana ili kufikia lengo. Anasema kwamba milango ipo wazi kwa msanii yeyote ambae angependa kufanya nae kazi.
Anamalizia kwa kuwataka wapenzi wa muziki wake waupokee wimbo mpya aliouachia mapema hivi punde, lakini amedokeza kwamba kwasasa anaandaa albamu, ambapo ikishakua tayari ataiweka wazi kwa ajili ya mashabiki wake.