Makamu wa rais wa zamani, Joseph Robinette Biden Jr., amechaguliwa kuwa rais wa 46 wa Marekani. Ushindi wa rais mteule Joe Biden, umetangazwa na vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani baada ya kufikisha kura 270 ambazo zinatakiwa kufikishwa kwa mgombea yeyote ili ashinde urais wa nchi hiyo.
Kutokana na ushindi huu, inamfanya kuwa rais mwenye umri mkubwa zaidi kuchaguliwa kuongoza taifa hilo tajiri la kiuchumi na kijeshi duniani.
Kamala Harris ambaye ni mgombea mwenza wa Joe Biden, anakuwa makamu wa rais wa kwanza mwanamke kwa Marekani na pia makamu wa rais wa kwanza ambaye sio mzungu bali ni mchanganyiko wa muhindi na mjamaica.
Ushindi wa Joe Biden kutoka chama cha Democratic, unahitimisha urais wa Donald J. Trump wa chama cha Republican ambaye anakuwa rais tano kwa nchi hiyo kupoteza uchaguzi baada ya kugombea kwa ajili ya kutaka kuongoza muhula wa pili wa urais.
Baada ya kutangazwa matokeo hayo, wamarekani kutoka miji mbalimbali wameingia mitaani kuanza kushangilia kuondolewa madarakani kwa rais Donald Trump.