Chicago
London
Dar Es Salaam
 
 

Mercedez Benz Ilimng'oa Nguza Marquis

News by : Juma Kasesa
 
06 Nov, 2011 15:13:46
 
//

 

 

KARIBU mpenzi msomaji wa Jamvi la Kulonga ikiwa ni Ijumaa nyingine tunakutana jamvini katika kujadili na kuchambua habari za muziki, wanamuziki na sanaa kwa ujumla. Katika Jamvi la Kulonga leo ningependa kuzungumzia kilichomfanya mmoja wa wapiga gitaa ya solo waliowahi kutamba miaka ya nyuma akiwa na bendi mbalimbali lakini zaidi akiwa na Orchestra Marquis De Zaire, Nguza Vicking, maarufu kwa jina la ‘Babu Seya’.

 

Jamvi la Kulonga limeamua kumzungumzia Nguza mwanamuziki mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutokana na uwezo aliokuwa katikati ya miaka ya 70 akionyesha uwezo mkubwa wa kulichezea gitaa hilo la solo anavyotaka ambapo aliifanya bendi aliyotamba nayo ya Orchestra Marques De Zaire kuwa maarufu na kuwa wapinzani wakubwa wa bendi nyingine ya muziki huo Orchestra Safari Sound iliyokuwa ikimilikiwa na mfanyabiashara wa Kichaga Hugo Kisima.

 

Kabla sijaingia kwa undani kujadili kile kilichonisukuma kuandika Jamvi hili ningependa kukueleza Nguza ndiye mwanamuziki aliyetunga jina la Marquis akishirikiana na mkongwe mwingine wa muziki huo Kikumbi Mwanza Mpango King Kiki, akiwa ni miongoni mwa wanamuziki waasisi wa bendi hiyo ambao walijaaliwa kipaji na Muumba Mbingu na ardhi katika fani ya muziki wa dansi kutokana na uwezo wa kutunga, kuimba na kulichezea gitaa la solo anavyotaka.

 

Jamvi hili linakujulisha wengi wanamfahamu Nguza kwa uwezo wake katika gitaa la solo akiwa na Orchestra Marquis De Zaire lakini kiukweli mwanamuziki huyo kipaji alichoanza nacho katika medani ya muziki wa dansi ni kupiga gitaa zito la besi.

 

Kwa sasa mwanamuziki Nguza na mwanae Papii Nguza maarufu kwa jina la Papii Kocha wanatumikia kifungo cha maisha gerezani baada ya kutiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa makosa mawili ya kubaka na kulawiti 2007.

 

Nguza ni mwanamuziki ambaye robo tatu ya nyimbo zilizovuma za Marquis ameshiriki yeye katika kupiga solo ambapo miongoni mwa nyimbo hizo ni ‘Wanaume wa leo’, ‘Clara’, ‘Mayasa’, ‘Wema wangu’, ‘Doubledoble’ ‘Ngalula’, ‘Makumbele’, ‘Mpenzi Luta’, ‘Mpenzi Scola’, ‘Karubandika’, ‘Seya’, ‘Tipwatipwa’, ‘Kisebengo’, ‘Wakati nilikuwa mdogo’ ‘Bi Sofia’, ‘Hali ngumu’, ‘Ni wewe pekee’, ‘Kibulwa’, ‘Huba wangu’, ‘Mapenzi sio masihara’, ‘Mabruki’, ‘Anjelu’,’Balimwacha’, ‘Kazi yangu Baharia’ na ‘Mapenzi ya pesa’.

 

Nikirudi katika kile kilichonisukuma kuandika Jamvi hili ni kwamba Nguza alitamba sana Marquis na kupata umaarufu tangu katikati ya miaka ya 70 ambapo ghafla mwaka 2000 alitangaza ghafla kujiunga Orchestra Safari Sound na kubadilisha mtindo iliyokuwa ikiutumia wa ‘Dukuduku’ chini ya Supreme Maestro Ndala Kasheba na kuja na ‘Rashikanda Wasaa’ na ‘Power Iranda’ ambapo alivuma na bendi hiyo kwa kutoa nyimbo mbalimbali.

 

Mmiliki wa Safari Sound, Hugo Kisima, aliamua kumchukua mwanamuziki huyo ili kuimarisha bendi hiyo baada ya aliyekuwa kiongozi wakati huo Kasheba na mtindo wake wa ‘Dukuduku’ kujiondoa baada ya mkataba wake kuisha na kuelekeza nguvu katika bendi yake binafsi ya Zaita Muzika ‘Wana Zuke Muselebende’ ambapo alimtwaa Nguza ambaye pia alikuwa akijulikana kwa jina la ‘Big Sound’ kwa kumnunulia Mercedes Benz ya rangi ya njano ambayo ilimfanya kupiga kambi ndani ya bendi hiyo.

 

Nguza alishirikiana na wanamuziki wengi kama Skasy Kasambula, Alex Etoto,Tino Masinge ‘Arawa’, Mhina Panduka ‘Toto Tundu’ na kutengeneza nyimbo kadhaa lakini bendi hiyo ilishindwa kuwika kulinganisha na awamu zingine zilizopita ambapo Kisima aliamua kuivunja bendi hiyo na kuelekeza nguvu kwenye biashara ya kuuza dhahabu ambapo alifungua sonara inayoitwa Safari Jewellers iliyopo Kariakoo jijini Dar es Salaam.

 

Orchestra Safari Sound ni bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mfanya biashara wa Kichaga kutoka Ushi Rombo, Mkoani Kilimanjaro aitwaye Hugo Kisima na maskani yake yalikuwa katika Ukumbi wake wa Safari Resort, Kimara na White House jijini Dar es Salaam, ikiwa imeasisiwa na wanamuziki wengi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) zamani Zaire.

 

Miongoni mwa waasisi wa bendi hiyo iliyokuwa na uhasama na bendi nyingine iliyokuwa na asili ya Congo ya Marquis De Zaire, walikuwa ni Mbombo wa Mbomboka, Twahiri Mohamedi, Mongastan, Alex Kababa Nkomba Motoo, Mpayo Kalenga na Zagalo.

 

Jamvi la Kulonga linajukulisha kuwa Safari Sound ilianza kuwika na katika medani ya muziki dansi ikitumia mtindo wa ‘Nyekese Paralise’ chini ya Mbombo wa Mbomboka, kabla ya kuibuka na ‘Masantula’ ambao uliasisiwa na waimbaji wakongwe King Kiki na Sony Chibanda na baadae ikawa chini ya ‘Supreme’ Maestro Ndala Kasheba ambaye alitamba na mtindo wa ‘Chunusi’ na ‘Dukuduku’ ukiwa ni dongo kwa wapinzani wao Marquis ikiwa ni jibu la mtindo wa bendi hiyo uliokuwa ukitamba wa ‘Ogelea Piga Mbizi’.

 

Baadhi ya wanamuziki waliowahi kuitumikia bendi hiyo kwa nyakati tofauti ni Tshibanda Sony, Dingituka Molay, Kabeya Badu, Skasy Kasambula, Monga Stanley Matuka Mwenda, Abel Baltazar, Joseph Mulenga, Muhidin Maalim Gurumo, Hasan Rehani Bitchuka, Kassim Rashid, Charles John Ngosha, mpiga dramu Chipembele Said na Shabani Dede.

 

Kwa nyakati tofauti bendi hiyo iliweza kutikisa medani ya muziki wa dansi kwa kutunga nyimbo kama ‘Mfakamanga’, ‘Dunia Msongamano’, ‘Manyara’ ‘Shukrani kwa Mjomba’, ‘Si ‘Wazuri Binadamu’, ‘Chatu Mkali’ ’Ford’ ‘ ‘Maudhi’ ‘Christina Moshi’, ‘Takadiri’, ‘Saleh’, ‘Pole Kaka Mudi’, ‘Uzuri wa Tausi’, chini ya waimbaji Skasy Kasambula, Kabeya Badru, Kalala Mbwembwe, Kibanda Ramadhani na Dingi Tukamulai.

 

Kwa wale wanaokumbuka enzi za ukumbi wa Safari Resort kama mzee wa Jamvi la Kulonga watakumbuka namna ukumbi huo ulivyokuwa ukifurika mashabiki kila Jumamosi, na DDC Magomeni Kondoa, kabla ya bendi hiyo kusambaratika mwanzoni mwa miaka ya tisini kutokana na mabadiliko yaliyofanywa na Kisima kuamua kuchanganya wanamuziki wenye asili ya Kongo na Watanzania wafanye kazi pamoja na jambo lililozua mtafaruku na kuwa chanzo cha kifo cha bendi hiyo.

 

Kwa leo nalikunja Jamvi. Kwa maoni na ushauri tuwasiliane: jkasesa@hotmail.com, 0715-629298

 

SOUCE: Tanzania Daima

 
 
 
 
 
Copyright © 2011 Bongo Radio. Subsidiary of Bongo Media Group. All Rights Reserved
Valid XHTML 1.0 Transitional